UTANGULIZI
Diwani ya Tanzanet ni Jarida la Jumuiya ya Watanzania duniani kote linakuwa Jukwaa kwa ajili ya Mashairi, Tenzi, Ngonjera na Tungo mbali mbali kwa lugha ya Kiswahili. Azma ya Diwani ya Tanzanet ni kuhamasisha Watanzania na Watumiaji wote wa lugha ya Kiswahili kujaribu kutunga, kueleza mambo mbali mbali kwa lugha fasaha, kishahiri, ikiwa pamoja na kueleza mambo mbali mbali yanayomhusu Matanzania na mazingira yake yaliolezwa kiasanii.
Diwani ya Tanzanet itaweza kufikisha tenzi, tungo, na mashiri mbali mbali kwa uwanja mpana zaidi ambao utasaidia kupanua mawazo na ufahsaha wa lugha na jinsi ya kuitumia kwa kufupisha maana iliyoelezwa katika sehemu mbali mbali wakati huo huo kufikisha ujumbe rasmi, bila kupoteza maana yake.
Diwani ya Tanzanet itakuwa uwanja wa kutoa mawaidha, mafumbo, kumueleza mtu sifa na tabia zake, kutabili hali ya wakati, kuonya, na kutoa mwanya kwa malumbano ya kishahiri. Wakati huo huo kukuza ufasihi wa lugha na kutoa nafasi ya kuendeleza utafiti na utenzi wa lugha ya kiswahili. Hii ikiwa na maana kuwa Diwani ya Tanzanet, inaweza kutoa mwanaya wa mashairi yale ambayo yanakiuka taratibu na kanuni zilizozoeleka za utaungaji wa mashairi ya Kiswahili, ili kuweze kuwa na nafasi ya mabingwa kujitokeza na kusahihisha yale wanayoyaona kuwa ni potofu na wakati huo huo kutoa uwanja na mpenyo mkubwa wa ukuaji wa Tenzi na Mashairi mbali mbali ikiwa pamoja na kuelimishana.
Aziz Ponary Mlima
Mratibu Toleo la Kwanza.
25 Februari 2002
|